SIFA ZA FASIHI SIMULIZI


(a)        Sifa ya utendaji 
          huifanya fasihi simulizi  kuwa hai. Utendaji unaambatana na masimulizi ya mdomo wa fanani na sikio la hadhira. Utendaji pia unaweza kuambatana na muziki au ishara za mwili ambazo fanani huziwasilisha kwa hadhira yake. Utoaji wa fasihi simulizi hutegemea sana matumizi ya  viimbo, shada, miliolio  (viigizi) na vifaa vingine vya semi. Panaweza pia kuwa na ishara zinazoonekana kama vile midomo kuchezeshwa na kubinuliwa, kukunja uso, kubinya macho, kugusa mabega na  misogeo mingine ya mwili, na kadhalika.

Mtendaji (fanani) ni muhimu sana katika fasihi simulizi inayoelemea katika utendaji. Mtendaji ndiye anayefanya mambo kama kuimba, kutamba, kusema na kadhalika. Wakati mwingine huyu hutunga tanzu za kifasihi simulizi na huziwasilisha kwa hadhira. Mara nyingi mtendaji hueneza kazi zilizokwisha tungwa na fanani wengine hapo zamani. Ni kwa njia hii fasihi simulizi huenezwa na kupokezana toka vizazi hadi vizazi.

(b)        Kuweko kwa hadhira 
         inayokabiliana na fanani (mtendaji) kunafanya kuwe na athari mbalimbali za kiuhusiano kati yao.  Kama utendaji wa fanani hauiridhishi hadhira, fanani anaweza kuirekebisha kazi yake na kuifanya iwe bora zaidi. Kipimo cha uzuri wa uwasilishaji wake kitatokana na athari inayojitokeza kwa hadhira yake. Wakati hadhira hiyo inapojishirikisha katika utendaji, kimsingi itaweza kupanua mbinu na nafasi ya welewa wa dhamira zinazoelezwa na fanani.

(c)        Suala la mazingira 
         pia ni la muhimu sana. Mazingira huathiri mara zote usanii wa tungo pamoja na maudhui yake. Kwa mfano ziko tungo ambazo kimsingi huambatana na matukio maalum. Aidha, hata kama tungo hizo zikipitwa na wakati, zinaweza zikabadilishwa na fanani ili kusadifu mazingira maalumu ya  wakati huo. 

   (D)      Suala la ujitegemeaji:
          Wakati mwingine, fasihi simulizi huwa na tabia ya kuwa na ujitegemeaji. Mara nyingi    fasihi   simulizi hujitegemea katika sanaa za ghabi (mf. muziki) na kuchota uhai wake kutokana na vitendo na vitabia vya fanani, toni ya muziki na kadhalika. Kutokana na tabia hii ya ujitegemeaji, fasihi simulizi ikiwekwa katika maandishi huonekana kuwa chapwa kwa sababu mambo kama vidoko, miondoko, na ngoma vinakuwa havimo. Vitu hivyo haviwezi kuhifadhiwa kimaandishi na kwa hivyo hii ndio sababu ya kujitofautisha na fasihi andishi; fasihi simulizi ina maisha, yaani ni hai.

 jiunge nasi bofya hapa ku-install application yetu swahiliform ili usisumbuke kuingia kwenye website yetu
Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment