Aina za Barua


Zifuatazo ni aina kuu za barua zinazoandikwa mara kwa mara:
·        Barua za Kirafiki:  Hizi ni barua wanazoandikiwa wazazi, marafiki, watani na wajuani. Hizi zina uhuru mkubwa katika kuziandika.  Hazidai utaratibu wa pekee sana.  Mtu huwa huru kuandika upendalo ilimradi halimvunjii mtu heshima yake.

Barua ya aina hii huandikiwa marafiki, na jamii. Huwa mwandishi anajuli kama kwa wale anaowaandikia kwa hivyo si lazima iwe na sahihi yake au majina (yake yote) kamili. Kwa kawaida barua hii inaanza kwa salamu. Huwa ina anwani ya mwandishi peeke. Mwishoni mwandishi huweza hata kuwatumia salamu watu wengineo anaowajua na wanaomjua.

(i)        Muundo wa Barua ya Kirafiki
                                                                                    Shule ya Msingi kibo,
Sanduku la Posta 120, 
MOROGORO. 
Agosti 3, 2005
Kwa Baba mpendwa,

Ni matumaini yangu kwamba hujambo, tangu tulipoachana. Je, majirani zetu huko nyumbani huwajambo? Mimi ni mzima, sina neno.

Madhumuni ya kukuandikia barua hii ni kukuarifu Maonyesho ya Kilimo ya Wilaya ya Namtumbo. Kila mwanafunzi anahitajika kulipa shilingi mia moja za kugharamia nauli, chakula na kiingilio. Nakuomba unitumie pesa hizi tafadhali Baba, ili niweze kuandamana na wenzangu.

Nisalimie Mama, ndugu zangu na wote wanaonifahamu. Kwa heri kwa sasa.

Ni mimi Kitinda-mimba wako,

Martha.

           
ZOEZI
1.            Wewe u mwanafunzi katika shule ya bweni. Mwandikie mama yako barua ya kumjulisha  siku ya kufungwa kwa shule, huku ukimuomba aje kukuchukua kwenda nyambani.

2.            Umefuzu katika mtihani wako. Ndugu yako anayefanya kazi Nairobi, alikuwa amekuahidi zawadi ,maalum, ukishapita mtihani huo. Sasa mwandikie barua, umuombe akuletee zawadi.

3.            Umepata habari kwamba rafiki yako alipatwa na ajali ya barabara. Kwa sasa amelazwa katika hospital kuu ya Mkoa wa Mashariki. Mwandikie barua ya kumpa pole na kumtakia apone haraka.

4.            Likizo ya mwisho wa mwaka imekaribia. Mwandikie Baba yako anafanya kazi katika nchi za mbali. Mwambie akuletee nguo mpya na aje kushiriki nanyi wakati wa Sikukuu.

5.            U mwanariadha mashuhuri sana. Umechaguliwa kuiwakilisha shule yako katika mashindano ya Wilaya. Mwandikie barua rafiki yako, umweleze vile ulivyoshiriki na kupata ushindi katika mashindano ya Kata.

·        Barua za Mwaliko:
   Unapoalikwa kwenye michezo, tafrija, mikutano ya vyama au kwenye midahalo, unaandikiwa barua za mwaliko yenye sifa kama ifuatavyo:
                               
(i)            Barua hizi sharti ziwe fupi na wazi.

(ii)         Zitaje tarehe, saa na mahali pa kukutania;

(iii)    Jina la mwalikaji na anwani yake kamili lazima itajwe;

(iv)    Aidha, jina la mwalikwa na kusudi la mwaliko na pengine vitu anavyopaswa kwenda navyo inapaswa vitajwe.

·        Barua za kazi na shughuli: 
  Barua zinazohusika hapa ni zile za kuomba kazi, kutoa ripoti ya kikazi, shughuli za kiserikali,  kichama na kidini.  Katika barua hizi kumbuka:
 (i)    Kutaja nambari au/ na tarehe ya barua zinazopaswa kurejewa;
 (ii)   Kichwa cha barua na aina ya shughuli unayotaka izingatiwe.         

·        Barua ya Kiofisi (Rasmi)
Barua ya aina hii huandikiwa Maafisa wa Serikali au Makampuni ya watu binafsi. Kwa   kawaida, maafisa hawa si lazima wamjue mwandishi. Barua rasmi, basi huwa na anwani ya mwandishi (upande wa juu, mkono wa kulia) na anwani ya anayeandikiwa, upande wa     kushoto. Anwani hufuatiwa na mtajo –  (kichwa cha habari). Barua hii huanza moja kwa           moja, bila salamu. Ujumbe pekee ndio unaoandikwa. Mwishoni, mwandishi huandika majina yake kamili (rasmi) na sahihi yake.
(ii)       Mfano/Muundo wa Barua Rasmi:
                                                                                                                  Shule ya Msingi kibo,
                                                                                                                   Sanduku la Posta 222,
                                                                                                                        MWANZA
                                                                                               
                                                                                                                     Agosti 3, 2005
            Mkurugenzi,
            Chama cha Wakuza Mboga,
            Sanduku la Posta 456,
            MWANZA


            KUH: UUZAJI WA MBOGA

            Ningependa kukujulisha ya kwamba Wanafunzi wangu wa Chama cha MOTCA wamekuza kabichi na karoti nyingi.

            Nakuomba utusaidie katika uuzaji wa mboga hizi ambazo kwa sasa tayari zimekomaa.

            Natumai utatusaidia uwezavyo.

            Ahsante.

            Wako mwaminifu,
            (Sahihi)

            Nsaji Peter Njarambaya
            MWALIMU MKUU


Anwani
Kama mwandishi na mwandikiwa wote wanapatikana katika nchi moja (Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Zambia, Malawi, nk.), basi anwani huandikwa ndani ya barua kama ifuatavyo:
                                                                                                             Shule ya Msingi kimawe,
                                                                                                               Sanduku la Posta 2222,
                                                                                                                         moshi.
                                                                                                                               
                                                                                                                   Agosti 3, 2005

lakini juu ya bahasha, yaani kule inakopelekwa barua, huandikwa kama ifuatavyo:

Mkurugenzi,
            Chama cha Wakuza Mboga,
            Sanduku la Posta 56,
            NAMTUMBO
Kama mwandishi na mwandikiwa wote wanapatikana katika nchi tafauti (anayeandika yuko Tanzania,  na anayeandikiwa yuko Kenya , Uganda , Zimbabwe , Zambia au Malawi, nk.), basi anwani huandikwa ndani ya barua kama ifuatavyo:

                                                                                                            Shule ya Msingi Mawezi,
                                                                                                             Sanduku la Posta 2222,
                                                                                                                         MWANZA.
                                                                                                                     TANZANIA
                                                                                                              Agosti 3, 2005
           
na juu ya bahasha, yaani kule inakopelekwa barua, huandikwa kama ifuatavyo:

Bwana
Paul Kipruto,
Chama cha Wakulima Langas,
Sanduku la Posta 146,
Eldoret,
KENYA

(iii)     Mfano wa Bahasha

Bwana
                        Paul Peter Simala,
                        Chama cha Wakulima Mumias,
                        Sanduku la Posta 123,
                        Eldoret,
                        KENYA

·        Barua za Biashara na Matangazo: Matangazo ya biashara magazetini ni ghali. Kwa hivyo, barua ziwe fupi na wazi ili zisimpotezee mfanyabiashara muda wake.
        
·        Simu: Kuna simu ya mdomo  na barua ya simu. Barua za simu ni fupi sana. Mtu huna fursa ya kueleza mengi au kuzungumza moja kwa moja na yule unayempelekea taarifa. Isitoshe barua za simu zatarajiwa kwenda haraka zaidi kuliko barua za kawaida.

Gharama ya kuilipia hukadirwa kwa idadi ya maneno yaliyoandikwa: maneno mengi, gharama kubwa, maneno machache, gharama ndogo.

Kwa ufupi, kuna barua ya kirafiki (kindugu) na barua ya kiofisi (rasmi).

Hatua za Kuangalia katika Barua
                       
Hatua zinazotakiwa kuchukuliwa wakati wa kuandika barua ni kama ifuatavyo:

(a)       Hatua ya Jumla:
(i)        Anwani ya mwandikaji, ndani ya barua,
(ii)       Anwani ya mwandikiwa iandikwe vema,  juu ya bahasha na pengine ndani ya barua pia;
(iii)     Tarehe,          
(iv)      Salamu (maamkio),
(v)       Barua yenyewe,
(vi)      mwisho wa barua.   
(vi)      Tumia karatasi na bahasha safi.    
(vii)    Juu ya bahasha ya mtumiwa barua, iwekwe stempu inayostahiki;
(viii)   Kama ni kifurushi, funga kamba kwa umbo la kukatana;
(ix)      Iwapo ni rejesta, chora mistari ya kukatana: moja wa wima na mwingine wa kulala katikati ya bahasha nyuma na mbele.

(b)       Hatua za Pekee:

(i)        Katika Barua za Kazi na Shughuli za Kiserikali:
Licha ya hayo yaliyotajwa katika (a) hapo juu,
·        Andika kichwa cha barua kinachotaja nia ya barua kwa sentensi
      moja fupi kabla ya maelezo ya barua yenyewe.
 
·        Barua nzima iwe fupi na wazi.

(ii)       Katika Barua za Biashara:             
            Pamoja na hayo yaliyotajwa katika (a) hapo juu,

·        Ongeza orodha ya vitu unavyoagizia.
·        Eleza jinsi ya kulipia iwapo ni kwa fedha taslimu, au malipo mara upokeapo vitu unavyoangiza yaani, (c.o.d }ikiwa na maana ya: (‘cash on delivery’} au iwapo ni kwa hundi.
 
(iii)     Barua za Simu
Mambo muhimu yanayotakiwa katika barua za simu ni:
    
·        Anwani kamili ya mtu yule unayempelekea simu.   
·        Toa taarifa kwa kifupi na wazi kwa maneno yasiyozidi kumi.
·         Kumbuka maneno yote yanaozidi kumi ya kwanza utatozwa zaidi.
·        Andika anwani ya mtuma simu.
·        Malipo taslimu ya nayotolewa palepale posta.

(iv)      Kutuma Fedha kwa Simu:
                        Ili kutuma fedha kwa simu zingatia mambo haya:

·        Lipa fedha taslimu kwa postamasta ofisini pamoja na ada ya kupelekea hizo fedha.

·        Dai risti ya kupelekea hizo fedha,  nayo uitunze ili uweze kuitumia kudai pesa zako hizo ikiwa zitapotea.
·        Mwandikie nduguyo unayempelekea hizo fedha ukimwarifu kwamba umemtumia fedha kiasi kadhaa, ili atakapoitwa posta na kuulizwa nani amemtumia fedha hizo, aweze kutaja jina lako na kupewa fedha zake.

(v)       Kutuma Fedha kwa Barua ya Rejesta:
Pamoja na kutumiwa fedha kwa njia ya simu, kupo pia kupelekewa fedha kwa barua ya fedha au rejesta. Hapa yafaa kukumbusha tu kwamba uchukuapo fedha zilizofika kwa rejesta, ifungue bahasha mbele ya postamasta na kuhesabu kwa uangalifu pesa zilizomo mbele yake, ili zikipungua au zisipokuwamo uweze kuanza madai mbele yake yeye akiwa shahidi.

(vi)      Kutuma taarifa kwa njia ya Faksi
Pamoja na simu leo kuna teknolojia za kisasa zaidi za kupashana habari. Nazo ni: Teleprinta, Teleksi, Faksi na Intaneti.

Kwa mfano, ukitaka kutumia taarifa kwa faksi, njia ambayo bado inayohifadhi siri kwa kiasi kikubwa, na inayochukua muda mfupi na gharama ndogo ni faksi.

            Unachotakiwa kukifanya ni                      
·        Kuandika taarifa yako kikamilifu kwenye karatasi nyeupe.
·        Kisha ipitishe hiyo karatasi yenye taarifa yako kwenywe mashine ya faksi ambayo itaituma taarifa yako huko unakotaka iende.
 
Huko iendako itapokelewa na faksi-mashine nyingine ambayo itatoa kwa maandishi nakala halisi (kopi) ya taarifa yako ambayo ataipokea uliyemtumia.

1.                  Tarehe zinaweza kuandikwa kama ifuatavyo:
(a)              3, Agosti, 2005
(b)              3 – 8 – 2005
(c)              3/8/2005

2.                  Anwani inaweza kuandikwa kama ifuatavyo:

(a)       Shule la Msingi Mbeya,
S.L.P. 343, 
                        MBEYA.

au

(b)       Shule ya Msingi MBEYA,
                        Sanduku la Posta 343,
                        MBEYA.



MAREJELEO



Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5 na 6.  Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.

 jiunge nasi bofya hapa ku-install application yetu swahiliform ili usisumbuke kuingia kwenye website yetu

Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

7 comments:

  1. UKURASA UMEPANGWA KIUTAALAMU KWELI ENDELEA NA MWANANGU WA DRS LA V ANAUTUMIA SANA KWENYW SOMO LA KISWAHILI

    ReplyDelete
  2. Asante sana kwa saada wako maana mitihani inaanza soon..

    ReplyDelete
  3. miye ojaka moses kutoka uganda

    makala haya yamenisaidia sana endeleeni vivyo hivyo
    ahsanteni sana

    ReplyDelete
  4. Je, neno Ndugu katika barua ya rasmi laweza kuwa ndio salamu yenyewe au vipi?

    ReplyDelete
  5. Insha kuhusu ugonjwa alivyo nasikia

    ReplyDelete