KUENEA KWA KISWAHILI KATIKA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO


Kwa mujibu wa maelezo ya Masebo na Nyengwine, (2002) Kiswahili kiliingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia karne ya 19. Nchi hiyo ilijipatia Uhuru wake kutoka Ubeligiji mwaka wa 1960.
Kiswahili kilianza kuenea kutoka Mashariki mwa nchi hiyo, kuelekea kandokando ya mto Kongo.

1   Sababu za Kuenea Kwa Kiswahili Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kabla ya Uhuru 1960
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zilizokifanya Kiswahili kienee katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla ya uhuru 1960:

(a)       Wafanyabiashara wa Kiarabu na watumwa wao ambao tayari walikuwa na umilisi katika kukizungumza Kiswahili, waliweka vituo vyao nchini Kongo kama walivyofanya Tanganyika. Na kama ilivyokuwa kawaida katika sehemu zote ambako wafanyabiashara waliendesha shughuli zao, Kiswahili kilikuwa ndicho lugha muhimu ya mawasiliano.

(b)       Wamishenari (wapelelezi) wa dini ya Ki-Kristo walianzia safari zao Zanzibar na pwani ya Tanganyika kuelekea bara ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Hawa walisaidia sio tu kuingiza lugha hiyo huko Kongo, bali pia kukiimarisha Kiswahili.

(c)       Kwa ajili ya mawasiliano ya kawaida katika sehemu nyingine, Kiswahili kilianzishwa kwa wenyeji, kama vile: jeshini, kwenye machimbo ya shaba, na Kisangani. Wenyeji walitakiwa kukitumia Kiswahili ili waweze kuwasiliana baina yao.          

(d)       Lugha ya Kufundishia - hususan panapo mwaka 1890, katika baadhi ya Shule, kama vile Seminari Ndogo ya Mpala huko Shaba, Kiswahili kilitumika kufundishia Sarufi ya Kilatini, Historia ya Kanisa, Hesabu na Jiografia.

(e)       Shirika la madini laamua kukitumia Kiswahili mwaka 1906 - Shirika la Madini lilianzishwa huko Katanga na kukusanya wafanyakazi kutoka sehemu mbalimbali nchini Kongo. Lugha yao ya mawasiliano ilikuwa ni Kiswahili, na hivyo kukifanya kiimarike na kuenea.

(f)        Wamishenari sio tu walichapisha vitabu na magazeti kwa Kiswahili, bali pia walikitumia katika shughuli zao, na kwa hivyo walikiimarisha sana nchini Kongo.

2   Juhudi za Kukidunisha Kiswahili Nchini Kongo Kabla ya Uhuru  
Kati ya mwaka 1930 – 1940 Serikali ya Kibeligiji ilijitahidi kukipinga Kiswahili kisienee na badala yake kutaka kukieneza Kifaransa na Kiflemishi.

3   Mbinu za Wabelgiji za Kukidunisha Kiswahili Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Baada ya Uhuru 1960                   
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zilizokifanya Kiswahili kienee katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo kabla ya Uhuru 1960 kama zilivyoelezwa na Saleh na Kasisa, katika Maganga 1997:159):

(a)       Sheria namba 174 ya tarehe 17-10-1962 iliyoleta mabadiliko ya kwanza ya nchi huru ilisema ‘Kifaransa ni lugha ya kufundishia tangu elimu ya msingi, na matumizi ya mojawapo ya lugha za Kikongomani (yaani Kizaire), kama yanasababishwa na umuhimu wa kielimu, yanatawaliwa na Katiba ya Kitaifa’.

(b)       Kiswahili, Kilingala, Kichiluba, Kikongo na lugha nyingine zote za kienyeji zilizokuwa zikitumiwa, zifutwe katika Elimu ya Msingi …

4      Sura ya Kiswahili Katika Zaire          
Kwa mujibu wa maelezo ya Saleh na Kasisa, katika. Maganga (1997:159), wanadai ‘Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya makabila 120 yenye lugha mbalimbali na inatumiwa na watu hao katika shughuli mbalimbali za kijamii’

Anaendelea kusema ‘… ni lazima kutofautisha lahaja tatu za Kiswahili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire). Kwanza, ni kile Kiswahili cha Zaire ya Juu  (italiki ni ya kwangu) ambacho pia hujulikana kwa jina la Kingwana. Pili, ni kile cha Kivu, na hasa kile cha Manyema, ambacho hujilikana kama Kiswahili Bora, na mwisho ni kile Kiswahili cha Shaba.’
Aidha, anaendelea kutufahamisha kwamba wanaisimu wa Zaire walifanya mabadiliko mwezi Mei, 1974 ambapo Kiswahili cha Zaire nzima kilipata sura mpya ambayo baadaye ilijulikana kama Kiswahili Bora au Kiswahili Sanifu chenye umbo moja kila mahali na katika matumizi yote… cha kuweza kufundishwa darasani kama somo mojawapo’.  

Madai haya ya mwisho kuhusu Kiswahili bora au Kiswahili sanifu chenye umbo moja kila mahali na katika matumizi yote cha kuweza kufundishwa darasani kama somo mojawapo si nchini Zaire tu ambayo kwa sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, bali pia katika nchi yo yote ambayo imekichagua Kiswahili kama ya lugha ya kutumia katika shughuli za kila siku darasani ama nyumbani au penginepo.
Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

1 comments:

  1. NATAMANI SASA KUKIFANYIA KAZI HIKI KIITWACHO KISWAHILI SANIFU CHA ZAIRE SASA. MAANA YANGU NI TUNA VISANIFU VIWILI AMBAVYO MICHAKATO YA USANIFISHAJI WAKE INAPISHANA KWA MUDA,WAHUSIKA NA MSINGI.
    PIA TUNAPASWA KUHAMU MWALIMU, HICHO KISANIFU CHA ZAIRE NDICHO KILE TUSIKIACHO KIKIBANANGWA BANANGWA KATIKA MATANGAZO NA MUZIKI WAO?

    ReplyDelete