KUKUA NA KUENEA KWA LUGHA YA KISWAHILI




3.1   Nadharia ya Ukuaji wa Lugha
Kuna mambo mbalimbali yanayofanya lugha yoyote ikue. Mambo hayo ni kama vile matumizi ya lugha katika shughuli mbalimbali kama vile:
·        Shughuli za utawala na kampeni za kisiasa.
·        Shughuli za kibiashara ndani na nje ya nchi.
·        Maswala ya Elimu.
·        Mikutano ya nchi (kitaifa) na kimataifa.
·        Shughuli mbalimbali za kiutamaduni, muziki, sherehe, nk.
·        Matumizi ya lugha katika vyombo vya habari kama vile magazeti, redio, televisheni, nk.

·        Urahisi wa lugha yenyewe katika kueleweka na kuweza kuchukua maneno ya kigeni au maneno ya utamaduni wa mataifa mengine bila mgogoro.


Urahisi huo wa lugha waweza kuwa katika:
(i)        Matamshi yake

(ii)       Msamiati
(iv)      Miundo
(v)       Maana-:mfano neno moja kuwa na maana zaidi ya moja, nk.
(vi)      Mwingiliano wa tamaduni mbalimbali na uhamiaji wa kigeni.
(vii)    Vita-husababisha kuchangamana kwa watu wengi pamoja na hivyo huweza kusababisha lugha ya utamaduni fulani kuenea na kukua haraka ukilinganisha na lugha za tamaduni nyingine.

(viii)   Usanifishaji-husababisha lugha fulani iteuliwe kutumika katika nyanja fulani kama elimu, utawala, biashara, nk. Na hivyo lugha hiyo hukua. Kutokana na usanifishaji ndipo tunapata lugha rasmi na lugha ya taifa.

Hivyo kukua kwa lugha ni hali ya kuongezeka kwa msamiati. Msamiati ni jumla ya maneno yanayotumiwa katika lugha fulani. Ili lugha yoyote ikue lazima msamiati wake ukuzwe.

Sababu za uundaji wa msamiati/maneno ni kama zifuatazo:
(a)       Kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo huchukua
            sura mpya kila siku.

(b)       Kwa ajili ya kuweza kutafsiri mengi kutoka lugha yako kwenda lugha ya kigeni au kutoka lugha ya kigeni kuingia katika lugha yako.

(c)       Ili kupata msamiati unaokubalika na shughuli mahsusi kama vile benki, forodhani, Jeshini,  nk.

(d)       Kwa ajili ya matumizi ya utamaduni wa watu wa taifa hili
            au hata taifa jingine. Jambo la muhimu ni kuona msamiati wa Kiswahili unaendelezwa ili kukidhi haja ya watumiaji wa Kiswahili katika kupokea maingiliano ya fani mpya za utamaduni wa kigeni.

(e)       Ili kukidhi msamiati wa masomo yote katika lugha yako, ambayo hapa ni Kiswahili.

 
KUENEA KWA KISWAHILI NCHINI TANZANIA
Lugha kusikika imeenea kama kuna ongezeko la watu wanaoitumia lugha yenyewe ndani ya nchi husika. Ongezeko hilo linakomaa kiasi cha kuvuka mipaka ya awali. Leo hii, Kiswahili kinazungumzwa si nchini Tanzania tu, bali pia nje ya mipaka yake: Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi na Msumbiji.

1   Kabla ya Ukoloni
Kuenea kwa Kiswahili nchini Tanzania kabla ya ukoloni kulikuwa wakati wa biashara ya waafrika wenyewe kwa wenyewe. Biashara hii, ilikuwa imeshamiri sana, si nchini Tanzania tu, bali pia katika upwa wote wa Afrika Mashariki. 
           
Wenyeji wa pwani na wenyeji wa bara, hususan Tanzania, walikuwa na mawasiliano ya muda mrefu kabla ya kufika wageni wa Kiarabu na Kizungu. Kulikuwa na safari za kibiashara baina ya Pwani na Bara zilizokuwa zikifanywa na Waafrika wenyewe. Katika safari hizo, watu wa Bara walikitumia Kiswahili cha pwani na kukieneza sehemu za Bara, sio tu wakati waliporejea makwao kuwataka hali ndugu na majirani zao waliowaacha kwa miaka kadhaa, bali pia wafanyabiashara hao walipokuwa wakifanya biashara zao na Waarabu. Kwa mantiki hiyo, ndio walioanza, bila kukusudia, kuieneza lugha ya Kiswahili kutoka Pwani hadi sehemu za Bara za Tanzania.

2       Tanzania Wakati wa Ukoloni
Wageni waliohusika walioshirikiana na Wenyeji katika kueneza Kiswahili nchini Tanzania wakati wa ukoloni walikuwa Waarabu, Waajemi, Wareno, Wajerumani na Waingereza. Sababu zilizowafanya waje Afrika Mashariki, husasani Tanzania, ni pamoja na kufanya biashara, kueneza dini na kutawala. 

3       Kutokana na Biashara
                                               
(i)        Waarabu
Kwa mujibu wa maelezo ya Nkwera (2003:119) Waarabu walifika Pwani ya Afrika Mashariki karne ya kumi. Walipofika hapa waliwakuta wenyeji wanazungumza Kiswahili, na kutokana na nia ya kueneza biashara yao, Waarabu wanajulikana sana kwa biashara, hususan biashara ya watumwa. Walishirikiana sana na watumwa katika dini, biashara na kuoana.Waarabu hao waliitumia lugha ya Kiswahili kila walipopita kufanya biashara yao. Lugha ilikuwa muhimu sana kwa mawasiliano kwa kila jambo walilofanya kati yao na wenyeji wao, hususan kwa kuwatumia watumwa wao.


Kwa kufanya hivyo, walijikuta wameeneza lugha ya Kiswahili.

Katika kuhakikisha kuwa lugha hii inafundishwa vyema na biashara inaendelea bila tatizo, Waarabu walianzisha vituo maalum kwa ajili ya biashara na wakati huo huo kufundisha dini ya Kiislamu. Vituo vya kibiashara kama vile Tabora na Ujiji vilikuwa na umuhimu mkubwa sana katika kueneza dini ya Kiislamu na Kiswahili hapa nchini.

(ii)       Wajerumani
Wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara na wakalazimisha Watanganyika kutoka Bara na Pwani kufanya kazi ya kulima katika mashamba hayo, hususan mashamba  ya Mkonge (katani).      Kwa kuwa walikuwa watu wa makabila mbalimbali, Kiswahili kilitumika sana katika mawasiliano baina yao. Na wale waliobahatika kurejea nyumbani, walisaidia kukieneza Kiswahili huko kwao.

4   Kutokana na Dini

(i)        Waarabu na Dini ya Ki-Islamu
Walipofika karne ya 10 waliwakuta wenyeji wakizungumza lugha zao za
Kibantu kikiwemo Kiswahili. Waarabu walipofika na dini ya Kiislamu walijikuta wakishirikiana na wenyeji wa upwa            huu katika mambo makuu matatu; Dini, biashara na kuoana.

Ili waweze kueneza dini yao vyema, Waarabu walijifunza kwa dhati lugha ya Kiswahili. Kwa vile walijishughulisha pia na biashara, Waarabu waliweza kujumuisha mambo mengi kwa mara moja.
                                         
(ii)      Wamishenari na Dini ya Ki-Kristo
Hawa walifika pwani ya Afrika Mashariki kabla ya utawala wa Wakoloni. Mashirika mbalimbali ya kidini yaliingia Afrika Mashariki katika nyakati tofauti tofauti. Mashirika haya ni “Roho Mtakatifu” toka Ufaransa mwaka 1868, White Fathers toka Ufaransa mwaka 1878, Church Missionary Society (CMS) ambalo liliongozwa na J.C. Krapf kutoka Ujerumani. Shirika hili mwaka 1876 liliandika sarufi ya kwanza ya Kiswahili cha Kimvita katika kitabu kilichoitwa Outlines of the Elements of Kiswahili Language with Specific Reference to the Kinika Dialect.

Pia mwaka 1845, Krapf alimpelekea katibu wa CMS orodha pana ya maneno (muhtasari) wa sarufi pamoja na tafsiri ya Injili ya Luka na Yohana ili kuwasaidia Wamishenari wengine ambao walikuwa wakiletwa Afrika ya Mashariki. Mwaka 1905 Misioni ya Magila walitoa kijitabu juu ya historia ya Wasambaa kilichoitwa Habari za Wakilindi. Makao makuu ya shirika hili yalikuwa Mombasa.
           
Shirika la Universities Mision to Central Afrika (U.M.C.A)     (Uingereza)           liliingia mwaka 1875 nchini, UMCA ilijishughulisha sana na kukiweka Kiunguja katika maandishi waka 1870 Askofu Edward Steere alichapisha toleo la kwanza la sarufi ya Kiswahili cha Kiunguja lililoitwa “A Handbook of the Swahili Language as Spoken at Zanzibar”. Pia walichapisha vitabu vya nyimbo na kamusi za Kiswahili na Kiingereza-Kiswahili kazi ya awali ya kuziandaa kamusi hizo ni ya Edward Steere, lakini ilikamilishwa na A. Madan na baadaye kurudiwa na F. Johnson aliyeandaa kamusi mbili A Standard English-Swahili Dictionary na Swahili English Dictionary ambazo zilitolewa mwaka 1939. UMCA walichapisha pia magazeti ya Msimulizi (1888), Habari za Mwezi (1876), Pwani na Bara (1910).

Kwa  ujumla wamisheni walijishughulisha sana na Kiswahili kwa sababu walikihitaji katika shughuli zao za kidini kwa kufanya hivyo walijikuta wanaikuza na kuieneza lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa kufuatana na uongezekaji wa vituo vyao nchini. Baadhi ya vituo hivyo ni Bagamoyo (1868), Magila (1864), Mpwapwa (1876), Ujiji (1877), Masasi (1876), Zanzibar (1860) na Ziwa Nyasa (1881).

5   Kutokana na Utawala

(i)        Kutokana na Utawala wa Wajerumani
Tunafahamishwa na Nkwera (2003:120) kwamba Wajerumani wameitawala Tanganyika kwa miaka thelethini (30) yaani (1885 – 1916)          kwa jina la Deutsch Ost Afrika (Afrika ya Mashariki ya Mjerumani).

Wajerumani walipoingia Tanganyika walikuta tayari kuna misingi mizuri ya lugha ya Kiswahili, Wamisheni walikuwa tayari wameandaa mfumo wa elimu na dini uliokuwa unatumia lugha ya Kiswahili. Kutokana na misingi hiyo utawala wa Kijerumani ulipoanzishwa nchini Kiswahili tayari kilikuwa kimeimarika.

Kwa hiyo, Wajerumani walikiona Kiswahili kuwa ni chombo muhimu sana kwa kuwasiliana na wananchi katika mawanda yafuatayo:
(a)       Kiswahili kilitumiwa na wamisionari kueneza Injili.

(b)       Katika Shule za watoto wadogo (Chekechea), Shule za Misingi na Shule za Kati (Middle Schools), Wamisionari walitumia Kiswahili kufundishia kuandika, kusoma, kuhesabu na kazi mbali mbali za ufundi, k.v. useremala, uashi na ufyatuaji mataofali.

(c)       Kwa upande wa Seriali, Kiswahili kilitumika kuelezea na kuenezea siasa ya Kijerumani na mipango ya Serikali kwa wananchi, na pia kuendeshea shughuli za  utawala.

            Kwa mantiki hii, Wajerumani walisisitiza sana kwamba Kiswahili kifundishwe mashuleni kote, na Kijerumani kifundishwe katika madarasa ya  Elimu ya Watu Wazima. Walilazimisha kila Akida afahamu Kiswahili barabara ili aweze kutumwa na kufanya kazi mahali popote, siyo tu katika sehemu aliyozaliwa na kukulia.
(e)       Wajerumani walijenga shule Tabora, Ujiji, Kilimatinde, Kasangu mwaka 1905 na hatimaye Bukoba, Mpwapwa, Iringa, Mwanza, Kilosa, Tukuyu na Moshi. Vyuo vya kufundishia Walimu vilianzishwa huko Tabora na Bukoba.

            Kutokana na Wajerumani kusisitiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli za utawala, shule,  kortini (mahakama) na hata katika kuwasiliana na wananchi, walisaidia sana kukieneza Kiswahili sehemu mbalimbali za Tanganyika.

 (ii)   Kutokana na Utawala wa Waingereza
Baada ya ujio wa Waingereza Tanganyika, juhudi mbalimbali zilifanywa katika kueneza Kiswahili nchini. Kwanza ilikuwa ni kuteua aina moja tu ya Kiswahili ambayo ingetumika katika nchi zote nne za Afrika Mashariki. Pia uwepo mtindo mmoja wa kukiandika. Hivyo mwaka 1928 mkutano ulifanyika Mombasa na walikubaliana kuwa nchi zote nne zitumie lugha ya aina moja yaani Kiunguja.

Mwaka 1929 Katibu wa halimashauri ya magavana wa Afrika Mashariki aliziandikia serikali nne kuhusu suala la kuanzishwa kamati ya lugha ya serikali zote nne na tarehe 1-1-1930 kukaanzishwa kamati iliyoitwa Inter-Territorial Language (Swahili) Committee ili ihusike na kusanifisha Kiswahili. Madhumuni ya kamati hiyo ya lugha ilikuwa kama ifuatayo:
(a)        Kuendeleza lugha moja kwa kupata maafikiano kamili katika mamlaka          ya Afrika Mashariki.
(b)        Kuleta ulinganifu kama itakavyoonekana, wa matumizi ya maneno yaliyoko na maneno mapya kwa kusimamia uchapaji wa makamusi ya mashule na mengineyo.
(c)        Kuleta ulinganifu wa sarufi kwa kuchapisha vitabu vya sarufi vilivyoafikiwa.
(d)        Kuwatia moyo na kuwasaidia waandishi ambao   ni wenyeji wa lugha ya Kiswahili.
(e)        Kuandaa vitabu vya Kiswahili vya kiada na vya ziada.
(f)         Kusahihisha lugha ya vitabu vya shule na vinginevyo ambavyo vimechapishwa mara masahihisho yanapohitajika.
(g)        Kutafsiri kwa Kiswahili vile vitabu vilivyochaguliwa  kwa ajili ya kutumiwa shuleni au kwa kusoma kwa ziada au kuvitunga moja kwa moja vitabu hivyo.
(h)        Kusoma na kuhakiki vitabu vya Kiswahili vinavyoshughulikiwa na kamati.
(i)          Kuwapa waandishi wa  vitabu maelezo ya taratibu za kufundishia za wakati uliopo katika nyanja mbalimbali.
(j)          Kujibu maswali yoyote kuhusu lugha ya    Kiswahili na fasihi yake.

Kamati hii ilitoa makamusi ya Standard Swahili-English-Swahili Dictionary. Mwaka 1935 kulianzishwa mashindano ya kuandika insha kwa Kiswahili katika shule za Kiafrika. Mwaka 1939 kukawa na mashindano ya waandishi wa vitabu. Vile vile kamati ilitoa kijarida kilichojulikana kwa jina la Bulletin of the Inter-Territorial Language (Swahili) Committee.

 (iii)    Kutokana na Vyombo Mbalimbali
Wakati wa utawala wa Mwingereza vyombo vilivyosaidia sana kueneza Kiswahili ni:

(a)    Elimu
Wakati wa Mwingereza Kiswahili kilitumika kufundishia shule za msingi, darasa la kwanza hadi la nne, na kilikuwa somo mojawapo hadi darasa la 12 katika shule za Waafrika.

(b)   Vyombo vya Habari
Vyombo vya habari vilivyojishughulisha sana na kukuza na kueneza Kiswahili ni magazeti, radio, nk.
·           Magazeti yaliyojishughulisha sana ni Masimulizi (1888), Habari za Mwezi (1894), Pwani na Bara (1910), Rafiki Yangu (1890), Habari za Leo (1954), Mwangaza (1923), Sauti ya Pwani (1940), Kiongozi (1950), Mamboleo, nk.

·           Chombo kingine cha habari ni radio Tanganyika ilianza matangazo kwa lugha ya Kiswahili mwaka 1950. Kwanza kama Sauti ya D.S.M. halafu baadaye kama Sauti ya Tanganyika.

(c)    Wakati wa Manamba
Utaratibu wa serikali za kikoloni ulikuwa ni kuzitenga sehemu fulani kwa ajili ya vibarua wa kufanya kazi katika mashamba hayo, mawasiliano yote yalifanywa kwa Kiswahili, na kwa njia hii kulikuwa na kukua na kuenea kwa Kiswahili kwa urahisi zaidi hapa nchini.

(d)    Suala la Jeshi (KAR)
Wanajeshi waliopigana katika vita mbalimbali walikuwa na nafasi ya kusafiri sehemu mbalimbali na kwa kuwa lugha yao ya mawasiliano ilikuwa ni Kiswahili, lugha hiyo iliweza kuenea kwa urahisi nchini.

(e)    Kampeni za Kisiasa
Baada ya vita ya pili ya dunia, mataifa mengi yaliyokuwa yanatawaliwa yalianza kudai uhuru wao, Afrika Mashariki nayo haikuwa nyuma.

Ingawa kulikuwa na makabila mengi yenye lugha tofauti, jambo lililowauganisha ilikuwa ni lugha ya Kiswahili, ambayo iliweza kueleweka na watu wengi. Lugha ya Kiswahili iliweza kuunganisha watu wa makabila tofauti katika mikutano mbalimbali iliyokuwa ikifanywa na vyama vya siasa nchini wakati huo.

Lugha ya Kiswahili ilisaidia sana katika kueneza siasa za TANU. Kiswahili ambacho leo ni lugha ya Taifa, kinatokana na lugha za kibantu. Kiswahili kinazungumzwa karibu na jamii zote katika Tanzania. Hivyo ilikuwa ni rahisi kuenea kwa TANU kwa watu wengi pasipo haja ya mkalimani. Hivyo mikutano mbalimbali ya kampeni za kisiasa ilisaidia sana kueneza Kiswahili nchini kwani mikutano mingi iliendeshwa kwa Kiswahili.


MAREJELEO

Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002),Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5 na 6.  Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.

Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.


jiunge nasi bofya hapa ku-install application yetu swahiliform ili usisumbuke kuingia kwenye website yetu

Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

8 comments:

  1. Asante.Ningependa kujua jinsi vyombo vya habari husaidia katika ukuaji wa fasihi ya watoto.

    ReplyDelete
  2. Kazi nzuri. Lakini pia ni vyema kama mtaweka marejeleo.

    ReplyDelete
  3. nikwanamna gani ndoa ilipelekea kukua kwa Kiswahili?

    ReplyDelete
  4. Maneno mwishoni wa kila sentensi haiwoneki

    ReplyDelete
  5. Kiswahili kilianza kutumika mwaka gani??

    ReplyDelete
  6. Nilitaka kujua kivip utalii umeweza kukuza kiswahili na utamaduni

    ReplyDelete