MISINGI YA UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI.



 MISINGI YA UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI.

Uhakiki ni uchunguzi au uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi. Uhakiki wa kazi yoyote ya fasihi unazingatia maeneo makuu mawili. Na Kazi za fasihi huhakikiwa kwa kutumia vigezo vikuu viwili maeneo hayo ni :
·                   MAUDHUI.
·                       FANI.

MAUDHUI.
Ni yale mambo yote ambayo yamemsukuma mwandishi /msanii kuandika kazi yake.Na pia  Maudhui ni mambo anayoyasema msanii kwa walengwa au hadhira yake. Katika kipengele cha maudhui mhakiki hana budi kuchambua mambo yafuatayo:
1.       DHAMIRA
2.       MIGOGORO.
3.       UJUMBE.
4.       FALSAFA.
5.       MTAZAMO.
6.       MSIMAMO.

DHAMIRA.
Ni suala linaloongelewa au kujadiliwa na mwandishi au msanii katika kazi ya sanaa. Ni kiini cha habari nzima iliyoandikwa au kusimuliwa.Ni wazo kuu au mawazo yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Kwa mfano Ukombozi wa mwanamke,Rushwa na Umuhimu wa elimu.

MIGOGORO.
Ni mivutano au mikinzamo inayojitokeza kutokana na misuguano ya kiuchumi,kisiasa kijamii na kiutamaduni . Ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili. Migogoro yaweza kuwa baina ya pande mbili au mtu binafsi. Kuna aina mbalimbali za migogoro. Aina hizo ni pamoja na :
Kisiasa, kiuchumi,kijamii na kinafsi.

UJUMBE.
Ni mafunzo au maadili yanayopatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi ili kuweza kupata ujumbe.  Ujumbe unaweza kutamka wazi au kwa kificho. Mhakiki hana budi  kujiuliza maswali yafuatayo:  mwandishi anatoa ujumbe gani kwa jamii?,anashauri nini?,je ujumbe huo unamhusu nani katika jamii?

FALSAFA.
Ni mwelekeo wa imani ya msanii ,mwandishi au msanii anaamini nini Mfano unaweza kubaini imani ya mwandishi Fulani kuhusu mwanamke au suala zima la maisha. Na pia unaweza kuijua vizuri falsafa ya mwaandishi kwa kusoma kazi zaidi ya moja za mwandishi anayehusika.

MTAZAMO.
Ni namna mwandishi anavyoona mambo , hapa mhakiki hana budi kubaini uyakinifu wa msanii. Mhakiki ajiulize je msanii ameandika mambo kwa kubuni au kudhani au kiuyakinifu au ameichunguza jamii kwa undani. Kwa mfano mtazamo wa kidini unaweza kumwongoza kuona kuwa, kila jambo nimapenzi ya mungu.

MSIMAMO.
Ni uamuzi wa kufuata jambo Fulani bila kujali kukubalika au kutokukubalika  kwa jambo hilo na jamii. Au ni maoni yake juu ya mambo mbalimbali anayoyaeleza kwenye kazi yake.

FANI.
Kipengele  cha fani hujumuisha mambo yafuatayo:
1.       MUUNDO.
2.       MTINDO.
3.       WAHUSIKA.
4.       MANDHARI.
5.       LUGHA.

MUUNDO.
Ni mtiririko au mpangilio wa visa/matukio ya kazi ya fasihi. Katika kuhakiki muundo msanii anapaswa kuchunguza kwa makini jinsi kazi ya fashii ilivyoundwa , namna tukio moja lilivyounganishwa na jingine,kisa kimoja kinavyounganishwa kisa kingine.Mhakiki achunguze mgawanyo wa sura katika riwaya.

AINA ZA MIUNDO.
Kuna aina kuu tatu za miundo ambazo msanii anaweza kutumia katika kuwasilisha kazi yake:
1.       Muundo wa moja kwa moja (MSAGO).
2.       Muundo rejeshi.
3.       Muundo rukia.

MUUNDO WA MOJA KWA MOJA.
Ni mfuatano wa matukio toka tukio la kwanza hadi mwisho huwa ni wa moja. Mhusika huanza kusimuliwa toka anazaliwa,anakua na hadi anakufa.

MUUNDO REJESHI.
Ni muundo wa kiuchangamano zaidi ambao hutumia urejeshi amakwa kumpeleka msomaji mbele au kumrudisha nyuma katika mpangilio wa matukio.

MUUNDO RUKIA.
Ni muudo ambao visa husimuliwa kwa kurukiana, muundo huu huwa na visa viwili ambavyo husimuliwa  kwa kurukiana, mwishoni visa hivyo huungana na kujenga kisa kimoja.

MTINDO.
Ni namna msanii anavyowasilisha kazi yake. Mtindo ni sifa mojawapo pambanua ambayo humtofautishaa msanii mmoja na mwingine. Aidha katika kipengele hiki cha mtindo mhakiki hulazimika kuchunguza yafuataayo: matumizi ya nafsi, matumizi ya masimulizi,monolojia au dialojiaa, matumizi ya barua, matumizi ya lugha nyingine nje ya kiswahili kama kiingereza.

WAHUSIKA.
Ni watu au viumbe vinavyowakilisha watu katika kazi za fashi. Uwakilishi huo huhusu hali halisi ya maisha jamii inayohusika. Aidha wahusika hubeba mawazo ya msanii na kubeba migogoro ya kijamii  inayozungumziwa katika kazi ya fasihi.

AINA ZA WAHUSIKA.
Kuna aina mbili za wahusika:
1.       Wahusika wakuu.
Ni mhusika wa muhimu kuliko wote. Huyu huonekana kuanzia mwanzo hadi mwisho  wa kazi ya fashi. Huyu ndiye hubeba dhamira au mawazo makuu ya msanii. 
2.       Wahusika wadogo.
Ni wahusika ambao wanaoonekana mara chache na kazi yao nikusaidia kumdhihirisha zaidi mhusika mkuu.

MANDHARI.
Ni sehemu ambapo au mazingira ambako matukio ya hadithi au masimulizi yanafaanyika .kazi fasihi hujengwa katika mazingira maalum ambayo huitwa mandhari. Mandhari katika kazi ya fashi husaidia kuleta hisia iliyokusudiwa. Mfano kama msanii anakusudia kuleta hisia ya woga humlazimu kuchukua mandhari ya woga kama msitu mnene, ngurumo za wanyama wakali.

LUGHA.
Ni kiungo muhimu sana katika kazi yoyote ile ya fasihi japokuwa lugha inayotumika katika kazi ya fasihi haina budi kuwa ni ya kisanaa zaidi ili kuweza kuibua hisia kwa hadhira yake.Ni lugha ambayo huwa na mvuto wa moja kwa moja kwa wasomaji wake kutokana na vionjo mbalimbali ambavyo msanii huvichanganya katika kumvuta msomaji kwa kuzingatia matumizi ya lugha fasaha, utenzi wa misamiati , matumizi ya misemo na tamathali za semi huongeza utamu na kufanya kuwa hai.

TAMATHALI ZA SEMI.
Ni semi ambazo hupamba lugha kwa kiasi kikubwa.Baadhi ya tamathalihizo ni pamojana
1.       SITIARI.
Ni  semi inayolinganisha matendo vitu au tabia tofauti bila kiunganisha.
 Mfano  Neema ni malaika.
2.       TASHBIHA.
Ni  semi zinazounganisha vitu kwa kutumia viunganishi kama NI,MITHILI,WA ,KAMA N.K 
kwa mfano Ana wembamba kama mlingoti.
3.       TASHIHISI.
Ni  semi ambazo vitu visivyokuwa watu hupewa sifa hizo.
 Mfano  Miti ililalamika siku  kucha kwa upepo mkali.
4.       MUBALAGHA.
Ni semi ambazo hukuza sana jambo kupita kiasi.
    Mfano Sauti yake inaweza kumtoa nyoka pangoni.
   Mfano alimlilia mumewe  hadi kukawa na bahari ya machozi.
5.       DHIHAKA.
Ni semi ambazo hutumia mafumbo.
6.       TAFSIDA.
Ni semi ambazo hupunguza ukali wa maneno.
Mfano Amejifungua badala ya amezaa.
7.       KEJELI.
Ni semi ambazo hutumia lugha ya kejeli katika kutoa ujumbe.
8.       TAKRIRI.
Ni semi ambazo baadhi ya maneno fulani hurudiwarudiwa kwa lengo la kuonesha msisitizo.
 Mfano kutwa,kucha,kutwa,kucha jambo ni hilohilo tu!
9.        MJALIZO.
Ni  semi ambazo huorodhesha vitu bila kutumia alama za mkato.


 jiunge nasi bofya hapa ku-install application yetu swahiliform ili usisumbuke kuingia kwenye website yetu
Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment