AINA ZA REJESTA




           
(i)     Rejesta za Mitaani
Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Lugha hii hudumu kwa muda mfupi tu, halafu hufifia. Wakati mwingine lugha hiyo hukubaliwa na jamii na kuweza kuingizwa katika msamiati wa lugha hiyo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke), “Nina waya” (sina pesa), “Kumwaga unga” (kupoteza kazi), umenoa” (umekosa), (mambo safi), n.k. Kwa ujumla lugha       ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka wa wazungumzaji wenyewe.

Mfano:
Ee bwana we! Maana hiyo Benzi ilikuja kitututu-wangu wangu! Bila kutazama mbele kunakuja nini, basi akamwingia babu wa watu-akamrusha     kama mpira,  alipofika chini, kwisha habari yake! Kichwa kama chapati. Simbaa wa mji watatumaliza...

(ii)       Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
-         Maofisini au mahali popote pa kazi
-         Mahakamani
-         Hotelini
-         Hospitalini
-         Msikitini
-         Kanisani  n.k

(a)        Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.

Mfano:
A:     Nani wali kuku
B:    Mimi
A:    Chai moja wapi?
B:    Hapa

Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”: ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.

(b)        Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti a lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitiza  usahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.

Mfano:
Wakili wa Utetezi:   Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Kenya?

Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Kenya na kukisoma) Ni kosa la uhaini.

Wakili wa Utetezi:   Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?

Kamishna Msaidizi:    Sijui. (Uhuru, 26 Agosti, 1982:4).

Kimsingi hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashtaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa maelezo.

(iii)     Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
-         Vijana wenye rika moja,
-         Wazee wenyewe,
-         Wanawake wenyewe,
-         Wanaume wenyewe,
-         Mwalimu na mwanafunzi,
-         Meneja na wafanyakazi wake,
-         Mtu na mpenzi wake, n.k.

(c)        Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.

Mfano:
Basi,  Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana’
‘Basi nilizamia infoo kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga’
‘Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa
noma kila mzamiaji’
Alikuwa mnoko kishenzi’
‘Akatema mkwala mbuzi, nikajibu kwa mkwala  dume....
akabloo mimi ndani’.

Maana ya Maneno
Wikiendi – Mwisho wa wiki.
Kibaridi –tulivu.
Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa.
Zinga la Mnuso –sherehe kubwa.
Saiti –sehemu.
Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni.
Noma – Hatari.
Mnoko kishenzi – kinaa sana
Mkwala mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).

Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.

Mfano mwingine wa wazungumzaji wa Kiswahili wa rika moja. Mzungumzaji Mkuu ni Chek Bob.

Yee! Mjumbe, degree kama degree mimi oyee tu. Nadhania umeiget fresh kuhusu nguvu-nguvu kazi au vipi?. Mimi ndo longtime niko hapa town bila Job nadunda na mensheni tu. Na vile vile ndo nina wiki ee tu tangu niopoe hiki kikwapa. Wewe mwenyewe ukikicheki kikwapa chenyewe waa! Sasa kwende nacho bush nishai au vipi mjumbe? Serikali yeneywe inatutia mikwala sana. Sasa shika hivi visimbi vya anda bee na kitembo (210) kusudi mimi nibane hapa hapa town. Hawa kinaa watilie mikwala mingi kwamba mimi ndo longtime nina Job. Kwani misheni hii ikijipa utaipata wewe mwenyewe mjumbe!. (Mfanyakazi Machi, 1988). Huu ni mfano mwingine wa kijana wa mjini, lakini anamweleza mjumbe hisia na maoni yake.


 (iv)     Lugha ya Kitarafa
Hiki ni Kiswahili cha tarafa fulani. Ukikisema katika tarafa nyingine huwa ni vigumu watu wa sehemu hiyo kuelewa unasema nini. Kwa ujumla ni Kiswahili ambacho kimeathiriwa na vilugha, yaani lugha-mama.
Kwa mfano:
Kiswahili cha Kiyao – John amenitona (amenifinya).
Kiswahili cha Kingoni – Mtambo mrefu (muda mrefu).
Kiswahili cha Kimakonde – Achante chana (asante sana).
Kiswahili cha Kinyakyusa – Kyama Kya Mapindusi (Chama cha Mapinduzi), n.k.

(v)       Kiswahili Rasmi/Sanifu
Ni msawazisho kutokana na vilugha vya lugha ya Kiswahili. Kiswahili hiki hukubaliwa na wengi katika nchi na ndicho kitumikacho katika shughuli za  kiserikali, kisiasa, elimu, uchumi, na vyombo vya habari hutumia lugha hii. Mtu akizungumza lugha rasmi ni vigumu kumtambua anatoka sehemu gani ya nchi. Kiswahili rasmi nchini Tanzania kinatokana na lahaja ya Kiunguja.

 jiunge nasi bofya hapa ku-install application yetu swahiliform ili usisumbuke kuingia kwenye website yetu

Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

5 comments:

  1. Mbona notes zenu zimekatwa hazionekana zote kwa nini hapa rekebisheni mitambo

    ReplyDelete
  2. aina za maneno iko wapi

    ReplyDelete
    Replies
    1. Angalia hapa
      https://www.google.com/url?sa=t&source=web&rct=j&opi=89978449&url=http://petermwiza.blogspot.com/2014/04/aina-za-sentesi.html%3Fm%3D1&ved=2ahUKEwi67K72x5WBAxUEQ_EDHYxrBRoQFnoECCQQAQ&usg=AOvVaw1YwQ8ICrkUqvmNY986ZYMX

      Delete
  3. Naipenda kiswahili

    ReplyDelete
  4. maswal[ ziko wapi

    ReplyDelete