1 Sababu Zilizokidunisha Kiswahili Nchini Rwanda Kabla ya Uhuru
Rwanda ni nchi ndogo
ya Afrika ya Kati ambapo Kiswahili huzungumzwa kidogo sana. Kwa mujibu wa
maelezo ya Maganga (1997:iv) sababu kubwa zilizokifanya Kiswahili kidunishwe na
kuzungumzwa au kutumika kidogo sana nchini Rwanda inatokana na historia ya
utawala wake wa jadi, kama ifuatavyo:
(a) Watawala
wa jadi hawakukubali watu waliokuwa wakizungumza lugha nyingine waingie na
kufanya biashara.
(b) Biashara
kutoka nje ya nchi ilikuwa ikifanywa na makabila ya jirani ambayo yalikuwa
yanaweza kuzungumza Kinyarwanda (lugha ya Taifa). Hawa ndio ambao waliruhusiwa
kuchukua bidhaa za Waarabu na za watu wengine wa nje ya nchi na kuziingiza
nchini Rwanda au kutoa bidhaa nje ya nchi.
(c) Wananchi
wa Rwanda hawakuweza kuzungumza Kiswahili hasa hasa kwa vile hawakuweza
kukutana kwa urahisi na watu wanaozungumza Kiswahili.
(d) Kiswahili
kimechelewa sana kuingia Rwanada. Inasadikiwa kuwa ni mnamo mwishoni mwa karne
ya 19 tu ndipo Kiswahili kilianza kuingia nchini Rwanda kwa mara ya kwanza
wakati wa utawala wa Kijerumani.
2 Sababu
Zilizokieneza Kiswahili Nchini Rwanda Kabla ya Uhuru
Sababu kubwa
zilizokieneza Kiswahili nchini Rwanda ni kama ifuatavyo:
(a) Wajerumani
waliwachukua baadhi ya watumishi kutoka Tanganyika, ambako idadi kubwa ya watu
walikuwa wakizungumza Kiswahili na kuja nao Rwanda kufanya kazi.
Ni katika kipindi hicho ndipo Kiswahili kilianza
kuingia nchini Rwanda na kuanza polepole kupata wazungumzaji.
(b) Mahubiri
ya Dini Ya Ki-Islamu
Wengi wa watumishi kutoka Tanganyika ambao Wajerumani
walikuja nao kufanya kazi Rwanda, walikuwa wakizungumza Kiswahil. Wengi wao
walikuwa Waislamu. Wakati wa utawala wa Wajerumani Rwanda na Tanganyika, lugha
ya mawasiliano ilikuwa ni Kiswahili katika shughuli za utawala.
Waislamu hawa pamoja na Waarabu walipokuwa
wameshaipata nafasi ya kuingia Rwanda, wakaanza kuihubiri dini yao kwa lugha ya
Kiswahili.
Baadhi ya Wanyarwanda walifuata Dini ya ki-Islamu na
wakaanza kuelewa Kiswahili.
(c) Mbeligiji
ambaye ndiye aliyekuwa mtawala wa Rwanda baada ya kwisha Vita ya Pili (1945) na
Mjerumani kuondoka Rwanda, hakukipenda Kiswahili; alikihusisha Kiswahili na
uislamu ambao ni adui mkubwa wa wakristo wakiwemo Wabelgiji.
(d) Shule
(i) Shule ya Mfalme Yuki Musinga na
Wasaidizi Wake
Kwa kuwa watawala wa jadi walipenda kuwasiliana na
Wajerumani ambao walikuwa wanatumia Kiswahili katika shughuli zao, Mwaka 1900
Mfalme Yuki Musinga alikubali kufundishwa kwa mara ya kwanza yeye na wasaidizi
wake lugha ya Kiswahili.
(ii) Shule
za Watawala wa Jadi
Kiswahili
kiliruhusiwa kufundishwa katika shule za watawala wa jadi; na kwa hivyo kupewa
nafasi ya kuena nchini Rwanda.
(iii) Baada
ya uhuru
Baada ya uhuru,
Serikali iliona umuhimu wa kukiimarisha Kiswahili nchini Rwanda. Kwa hivyo,
mwaka 1976/77 Kiswahili kikaanza tena kufundishwa katika Shule za Sekondari na
katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Nchini Rwanda, lugha ya Kiswahili ilifundishwa na
walimu kutoka Tanzania.
(iv) Juhudi za Wizara ya Elimu ya Taifa
Kutokana na mpango
wa kufundisha Kiswahili katika shule za sekondari, Wizara ya Elimu ya Taifa
ilianzisha kitengo cha kiswahili katika Taasisi ya Elimu ili kiweze
kushughulikia vema ufundishaji na ukuaji wa Kiswahili.
Kazi ya kitengo cha
kiswahili ni kutayarisha muhtasari, kuandika vitabu vya kufundishia, pamoja na
ukaguzi wa Kiswahili katika shule za sekondari.
(v) Redio Rwanda
Mnamo mwaka 1961
Redio Rwanda ilianza kutangaza baadhi ya vipindi kwa lugha ya Kiswahili.
Vipindi hivi ni kama vile: ‘Taarifa ya Habari’, ‘Salamu za Wasikilizaji’,
‘Matangazo ya Mpira’, ‘Ulimwengu Tuishio, na vingine vya kuelimisha wananchi.
3
Matatizo Yaliyokabili Kuenea kwa Kiswahili
Nchini Rwanda Baada ya Uhuru
Kwa uchache,
matatizo husika ni:
(a) Uchache wa walimu – shule nyingine za
sekondari hazikuwa na walimu wa
Kiswahili.
(b) Kiburi
cha Wanyarwanda - Wananchi wa Rwanda walikuwa
na kiburi, pengine mpaka leo; hawatilii maanani suala la kujifunza Kiswahili
kwa sababu ya kuogopa kwamba Kinyarwanda,
lugha yao ya Taifa, ingemezwa na Kiswahili.
(c) Wanyarwanda
wanazihusudu sana lugha za Wazungu, hususan Kifaransa, Kiflemishi na Kiingereza
kuliko lugha ya Kiafrika, hususan Kiswahili.
(d) Uchache wa vitabu vya Kiswahili
ulichangia na bado unachangia kwa kiasi kikubwa sana katika kupunguza kasi ya
kuenea kwa Kiswahili nchini Rwanda.
0 comments:
Post a Comment