AINA ZA INSHA



            INSHA/UTUNGAJI
Insha au Utungaji ni maandishi yanayoeleza habari juu ya kitu, mtu au jambo fulani. zipo aina mbili kuu za insha: insha za maelezo, na insha za mazungumzo. 
           

    Aina za Insha

 (i)       Insha za Maelezo
            Aina hii ya insha inajumuisha:
            (a)       Masimulizi ya mambo yaliyotokea (visa).
            (b)       Hadithi za kubuni
            (c)       Maelezo kuhusu au kutokana na msemo au methali fulani.

(ii)       Insha za Mazungumzo
            Aina hii inajumuisha:
            (a)       Mijadala
                       
            Katika insha ya kujadili, huwa kuna mambo mawili au zaidi;

Mwandishi anaweza kuzungumzia pande zote mbili, halafu atoe uamuzi wake. Lakini pia mwandishi ana uhuru wa kuchagua upande mmoja, ama wa kuunga mkono au kuipinga anwani aliyopewa, na kuzungumzia upande huo huo hadi mwisho.    

            (b)       Mazungumzo/Tamthiliya

Insha za aina hii huwa na mzungumzaji zaidi ya mmoja. Insha hizi pia zinajulikana kama insha za kujibizana. Mmoja akizungumza, naye mwenzake        humjibu apo hapo.

   Sehemu za Insha
Insha yo yote huwa na sehemu tatu muhimu:
                       
(i)        Mwanzo
Mwanzo wa Insha unakuwa kama salamu. Inafaa uwe wa kuvutia ili msomaji awe na hamu ya kuendelea kuisoma insha hiyo. Katika hatua hii, mwandishi hueleza maana ya mada/anwani/kichwa alichopewa. Endapo methali ni kichwa cha Insha, mwandishi ataeleza (i) maana ya juu, (ii) maana ya ndani, na (iii) matumizi ya methali aliyopewa katika jamii husika.

Endapo ni Insha ya mjadala, baada ya kueleza maana ya mada, mwandishi ataeleza kama anaunga mkono au ataupinga mjadala. Lakini pia anaweza kuamua kutoa maelezo ya pande zote mbili na halafu atoe uamuzi wake.

(ii)       Maudhui
Hii ni sehemu muhimu sana katika zoezi nzima la kuiandika Insha; ni kiini cha Insha. Ni sehemu ambayo ina aya kadhaa, na kila aya hujitosheleza kwa kila kitu katika kulielezea jambo moja tu au hoja  moja tu.
Wingi wa aya hutegemea wingi wa maudhui aliyonayo mwandishi wa kichwa cha Insha. Urefu wa aya hutegemea uwezo wa mwandishi wa kufafanua wazo linalozungumziwa. Kwa mfano, endapo ni Insha juu ya Maumbile ya Ng’ombe, aya moja inaweza kuwa juu ya kichwa cha ng’ombe. Ayah  inaweza kuwa ndefu kuliko aya kuhusu shingo au mkia wa ng’ombe.   
 (iii)    Hitimisho
Hitimisho ni aya ya mwisho ya Insha ambayo inaelezea muhtasari wa maudhui yote yaliyoelezwa katika Insha nzima.

(a)    Endapo ni Insha ya Mjadala, mwandishi anatoa uamuzi wake baada ya  kutoa maoni kuhusu pande zote mbili.

(b)    Endapo ni Insha ya Methali, mwandishi anaweza kusisitiza maana na matumizi ya methali, huku akitoa methali nyingine zenye maana sawa au maana kinyume na maana ya methali ya Insha. 

     Jinsi ya Kuandika Insha
(a)    Soma kwa makini mada/kichwa/anwani uliyopewa zaidi ya mara moja, ili uielewe vizuri.
                       
(b)    Ifikirie mada/kichwa/anwani kwa muda.

(c)    Yaandike mambo muhimu yatakayokuongoza katika kuiandika nsha             
 (d)   Yapitie mambo hayo muhimu ili uhakikishe kwamba yanaenda sawa na anwani: endapo kuna mambo ambayo hayafai, yaondoe; endapo kuna nyongeza, iandike.

(e)    Andika methali, misemo na nahau ambazo unadhania zinaweza kukufaa katika uandishi wa Insha yako.

(f)     Iandike Insha yako huku ikizingatia kwamba:
(i)     Aya ya Kwanza  =         Mwanzo

(ii)    Aya ya Pili           =         Kidokezo cha kwanza.
        
(iii)  Aya ya Tatu         =         Kidokezo cha pili.

(iv)   Aya ya nne          =         Kidokezo cha tatu. nk.

(iii)  Aya ya Mwisho  =         Hitimisho.

(g)    Isome Insha yako huku ukirekebisha makosa ya:
(i)     Tahajia
(ii)    Sarufi

  Miundo Mbali Mbali ya Insha

(i)        Kujibu Maswali ili Kuandika Insha
Katika muundo wa aina hii ya kuandika Insha, maswali yanayoulizwa lazima yatoemajibu ambayo yatasaidia kueleza habari kamili ya mtu, kitu, au jambo fulani. Kwa mfano:
(a)    Shughuli za Mwanafunzi/Mtu kunzia asubuhi anapoamka hadi usiku anapokwenda kulala.
        
(b)    Mifugo

(c)    Mmomonyoko wa Udongo

(d)    Nchi yetu, nk.

(ii)    Kujaza Nafasi ili Kuandika Insha
Insha yote huwa imesha kuandikwa isipokuwa tu kwenye sentesi fulani fulani za aya kumeachwa nafasi ya kujaza neno, kirai au kishazi kizima ambacho mwanafunzi anatakiwa akijaze ili kuleta maana kamili inayokubalika katika mtirirko mzima wa insha yenyewe.

(a)    Kukamilisha insha ambayo umepewa mwanzo wake

(b)    Kukamilisha insha ambayo umepewa mwisho wake

(c)    Insha za methali

Muundo wa Insha za aina hii ni kama ifuatavyo
(a)    Andika maana ya nje na ya ndani inayohusu methali uliyopewa:
(b)    Eleza mfano wa kisa (visa) vinavyothibitisha ukweli wa maelezo ya               methali.

(vi)      Insha za Kawaida
Zipo aina mbili za insha za kawaida:
               
(a)        Insha-Hadharishi – ni zile ambazo inafaa mwandishi awe mwangalifu katika kueleza yanayohusu vitu au mambo anayoyaelezea kwa sababu hivi ni vitu au mambo ambayo maudhui yake yanajulikana kwa watu wengi. Kwa mantiki hiyo, insha hizi hazimpi mwandishi fursa ya kubuni maelezo yake binafsi.

(b)        Insha-Huruni insha ambazo masharti yake ni kinyume na  yale ya Insha- Hadharishi. Katika uandishi wa insha-huru, mwandishi ana fursa yote ya kujieleza apendavyo. Anaweza hata kuandika mambo ya kubuni (uwongo); lakini ingemfaa mwandishi, kama angechopeza chembechembe za ukweli katika maelezo yake yaliyokithiri urongo ili insha yake angalau iwavutie wasomaji wake walio wengi wenye kuishi katika imani inayotawaliwa na kweli.

(vii)     Insha Zinazotokana na Picha
Katika insha za aina hii, mwandishi anapewa picha kadhaa zinaelezea kisa kwa ukamilifu wake. Kutokana na picha hizo, unatakiwa kuziandika sentesi kadhaa ambazo zitakuongoza katika kuikamilisha insha yako, kwa mfano:




            Malengo ya Insha/Utungaji
Somo la Insha/utungaji linalenga kumpa mwanafunzi mazoezi ya kutunga habari yeye mwenyewe, na jinsi ya kuziwasilisha habari zake kwa watu wengine kwa njia ya mazungumzo au maandishi. Somo hili linashughulikia vipengee vitatu: mazungumzo,  kuandika, kusoma, kufahamu na ufupisho (muhtasari). 

Jinsi ya kuyaendesha ni ile ile katika vidato vyote, tofauti ni katika viwango vya mifano itakayochaguliwa kushughulikiwa.

(i)      Mazungumzo
Shabaha ya somo hili ni kumfunza mwanafunzi kuzungumza na wenzake,  aidha kuhutubia hadharani, kujadili hoja, nk. kwa lugha fasaha, bila woga, akaeleweka.

(a)      Hotuba
Kuzungumza ni kipawa cha mtu kuweza kuwasiliana na wenzake. Kuna mazungumzo ya ishara, hasa baina ya watu bubu na mazungumzo ya mdomo. Hotuba ni mazungumzo  yaliyotayarishwa kwa muda mrefu au mara ile ile ili kutolewa mbele ya watu. Hotuba safi haina budi kuwa na mambo yafuatayo:
·        Ukweli wa habari na taarifa.
·        Ufasaha wa lugha ipate kupendeza na kueleweka vizuri.
·        Nidhamu, yaani adabu njema ya mzungumzaji mwenyewe asimamapo mbele za watu .
·        Mantiki nzuri, yani mfuatano mzuri wa mawazo na fikra.
·        Sauti ya kusikika wazi pamoja na ishara zinazoeleweka iwapo hotuba inatolewa mbele ya watu.  Ishara siyo za lazima iwapo hotuba inatolewa kwa njia ya redio.

Hotuba zaweza kugawanywa kwa misingi mbalimbali.  Baadhi ya misingi hiyo ni:
·        Urefu wa Muda wa Matayarisho: Kulingana na uzito wa mada za hotuba zenyewe matayarisho huwa ni ya muda mrefu kwa mada nzito, lakini huwa ni ya muda mfupi kwa hotuba zenye mada nyepesi. Aghalabu, hotuba za dharura huwa na mada nyepesi nyepesi,  yaani zinazotolewa papo  kwa papo bila ya kupata muda mrefu wa kuziandaa.

·        Aina za Hotuba: Ziko aina nyingi za hotuba. Baadhi yake ni:
(i)             Hotuba na Mafundisho ya Kidini; aghalabu, hizi hutolewa miskikitini, makanisani, kwa njia ya redio; lakini pia popote penye mkusanyiko wa waumini husika.
(ii)          Hotuba za Kisiasa na Kiserikali:  Kwa mfano; matangazo ya taarifa za kiserikali na chama, fafanuzi za maazimio au sheria, n.k.
(iii)        Mihadhara au Masomo ya Darasani:  Hizi ni hotuba au mafundisho ya Mwalinu shuleni hasa anapofundisha kundi kubwa la wanafunzi, na hasa wanachuo wa vyuo vikuu.

·        Nia ya mzungumzaji katika kuzitayarisha hotuba:

      Mzungumzaji au mhutubiaji hujiwekea lengo la hotuba yake:
(i)             Kuna hotuba za kuhimiza na kualika watu kutenda jambo fulani;
(ii)          Kuna hotuba za kupasha habari ya furaha au ya simanzi;
(iii)        Kuna hotuba za kushukuru,  kukaribisha wageni, kupongeza na kutoa hongera, kumliwaza na kumfariji mwenye huzuni na masikitiko,
(iv)        Aidha, kuna hotuba za kushutumu na kukaripia. 



MAREJELEO



Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5 na 6.  Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.
Share on Google Plus

About Se

mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo mwanza Tanzania ni miongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufaulu wa somo hili. tupo mwanza Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua
    Blogger Comment

9 comments: