INSHA/UTUNGAJI
Insha au Utungaji ni maandishi yanayoeleza habari juu ya kitu, mtu au
jambo fulani. zipo aina mbili kuu za insha: insha za maelezo, na insha za
mazungumzo.
Aina za Insha
(i) Insha za Maelezo
Aina hii ya insha inajumuisha:
(a) Masimulizi ya mambo yaliyotokea (visa).
(b) Hadithi za kubuni
(c) Maelezo kuhusu au kutokana na msemo au
methali fulani.
(ii) Insha za Mazungumzo
Aina hii inajumuisha:
(a) Mijadala
Katika insha ya
kujadili, huwa kuna mambo mawili au zaidi;
Mwandishi anaweza kuzungumzia pande zote mbili, halafu
atoe uamuzi wake. Lakini pia mwandishi ana uhuru wa kuchagua upande mmoja, ama
wa kuunga mkono au kuipinga anwani aliyopewa, na kuzungumzia upande huo huo
hadi mwisho.
(b) Mazungumzo/Tamthiliya
Insha za aina hii huwa na mzungumzaji zaidi ya mmoja. Insha hizi pia
zinajulikana kama insha za kujibizana. Mmoja akizungumza, naye mwenzake humjibu apo hapo.
Insha yo yote huwa na sehemu tatu
muhimu:
(i) Mwanzo
Mwanzo wa Insha unakuwa kama salamu. Inafaa uwe wa kuvutia ili msomaji
awe na hamu ya kuendelea kuisoma insha hiyo. Katika hatua hii, mwandishi
hueleza maana ya mada/anwani/kichwa
alichopewa. Endapo methali ni kichwa
cha Insha, mwandishi ataeleza (i) maana ya juu, (ii) maana ya ndani, na (iii)
matumizi ya methali aliyopewa katika jamii husika.
Endapo ni Insha ya mjadala, baada ya kueleza maana ya mada, mwandishi
ataeleza kama anaunga mkono au ataupinga mjadala. Lakini pia anaweza kuamua
kutoa maelezo ya pande zote mbili na halafu atoe uamuzi wake.
(ii) Maudhui
Hii ni sehemu muhimu sana katika zoezi nzima la kuiandika Insha; ni
kiini cha Insha. Ni sehemu ambayo ina aya kadhaa, na kila aya hujitosheleza kwa
kila kitu katika kulielezea jambo moja tu au hoja moja tu.
Wingi wa aya hutegemea wingi wa maudhui aliyonayo mwandishi wa kichwa
cha Insha. Urefu wa aya hutegemea uwezo wa mwandishi wa kufafanua wazo
linalozungumziwa. Kwa mfano, endapo ni Insha juu ya Maumbile ya Ng’ombe, aya
moja inaweza kuwa juu ya kichwa cha ng’ombe. Ayah inaweza kuwa ndefu kuliko aya kuhusu shingo
au mkia wa ng’ombe.
(iii) Hitimisho
Hitimisho ni aya ya mwisho ya Insha ambayo inaelezea muhtasari wa
maudhui yote yaliyoelezwa katika Insha nzima.
(a) Endapo ni Insha ya Mjadala, mwandishi anatoa uamuzi wake baada ya
kutoa maoni kuhusu pande zote mbili.
(b) Endapo ni Insha ya Methali, mwandishi anaweza kusisitiza maana na
matumizi ya methali, huku akitoa methali nyingine zenye maana sawa au maana
kinyume na maana ya methali ya Insha.
Jinsi ya Kuandika Insha
(a) Soma kwa makini mada/kichwa/anwani uliyopewa zaidi ya mara moja,
ili uielewe vizuri.
(b) Ifikirie mada/kichwa/anwani kwa muda.
(c) Yaandike mambo muhimu yatakayokuongoza katika kuiandika nsha
(d) Yapitie
mambo hayo muhimu ili uhakikishe kwamba yanaenda sawa na anwani: endapo kuna
mambo ambayo hayafai, yaondoe; endapo kuna nyongeza, iandike.
(e) Andika methali, misemo na nahau ambazo unadhania zinaweza kukufaa
katika uandishi wa Insha yako.
(f) Iandike Insha yako huku ikizingatia kwamba:
(i) Aya ya Kwanza = Mwanzo
(ii) Aya ya Pili = Kidokezo cha kwanza.
(iii) Aya ya Tatu = Kidokezo cha pili.
(iv) Aya ya nne = Kidokezo cha tatu. nk.
(iii) Aya ya Mwisho = Hitimisho.
(g) Isome Insha yako huku ukirekebisha makosa ya:
(i) Tahajia
(ii) Sarufi
Miundo Mbali Mbali ya Insha
(i) Kujibu Maswali ili
Kuandika Insha
Katika muundo wa aina hii ya kuandika Insha, maswali yanayoulizwa
lazima yatoemajibu ambayo yatasaidia kueleza habari kamili ya mtu, kitu, au
jambo fulani. Kwa mfano:
(a) Shughuli za Mwanafunzi/Mtu kunzia asubuhi anapoamka hadi usiku
anapokwenda kulala.
(b) Mifugo
(c) Mmomonyoko wa Udongo
(d) Nchi yetu, nk.
(ii) Kujaza Nafasi ili Kuandika Insha
Insha yote huwa imesha kuandikwa isipokuwa tu kwenye sentesi fulani
fulani za aya kumeachwa nafasi ya kujaza neno, kirai au kishazi kizima ambacho
mwanafunzi anatakiwa akijaze ili kuleta maana kamili inayokubalika katika
mtirirko mzima wa insha yenyewe.
(a) Kukamilisha
insha ambayo umepewa mwanzo wake
(b) Kukamilisha
insha ambayo umepewa mwisho wake
(c) Insha za
methali
Muundo wa Insha za aina hii ni kama ifuatavyo
(a) Andika maana ya nje na ya ndani inayohusu methali uliyopewa:
(b) Eleza mfano wa kisa (visa) vinavyothibitisha ukweli wa maelezo ya
methali.
(vi) Insha za Kawaida
Zipo aina mbili za insha za kawaida:
(a)
Insha-Hadharishi
– ni zile ambazo inafaa mwandishi awe mwangalifu katika kueleza yanayohusu vitu
au mambo anayoyaelezea kwa sababu hivi ni vitu au mambo ambayo maudhui yake
yanajulikana kwa watu wengi. Kwa mantiki hiyo, insha hizi hazimpi mwandishi
fursa ya kubuni maelezo yake binafsi.
(b)
Insha-Huru – ni insha ambazo masharti yake ni
kinyume na yale ya Insha- Hadharishi.
Katika uandishi wa insha-huru, mwandishi ana fursa yote ya kujieleza apendavyo.
Anaweza hata kuandika mambo ya kubuni (uwongo); lakini ingemfaa mwandishi, kama
angechopeza chembechembe za ukweli katika maelezo yake yaliyokithiri urongo ili
insha yake angalau iwavutie wasomaji wake walio wengi wenye kuishi katika imani
inayotawaliwa na kweli.
(vii) Insha Zinazotokana na
Picha
Katika insha za aina hii, mwandishi anapewa picha kadhaa zinaelezea
kisa kwa ukamilifu wake. Kutokana na picha hizo, unatakiwa kuziandika sentesi kadhaa
ambazo zitakuongoza katika kuikamilisha insha yako, kwa mfano:
Malengo ya Insha/Utungaji
Somo la Insha/utungaji linalenga kumpa mwanafunzi mazoezi ya kutunga
habari yeye mwenyewe, na jinsi ya kuziwasilisha habari zake kwa watu wengine
kwa njia ya mazungumzo au maandishi. Somo hili linashughulikia vipengee vitatu:
mazungumzo, kuandika, kusoma, kufahamu
na ufupisho (muhtasari).
Jinsi ya kuyaendesha ni ile ile katika vidato vyote, tofauti ni katika
viwango vya mifano itakayochaguliwa kushughulikiwa.
(i) Mazungumzo
Shabaha ya somo hili ni kumfunza mwanafunzi kuzungumza na wenzake, aidha kuhutubia hadharani, kujadili hoja, nk.
kwa lugha fasaha, bila woga, akaeleweka.
(a) Hotuba
Kuzungumza ni kipawa cha mtu kuweza kuwasiliana na wenzake. Kuna
mazungumzo ya ishara, hasa baina ya watu bubu na mazungumzo ya mdomo. Hotuba ni
mazungumzo yaliyotayarishwa kwa muda
mrefu au mara ile ile ili kutolewa mbele ya watu. Hotuba safi haina budi kuwa
na mambo yafuatayo:
·
Ukweli wa
habari na taarifa.
·
Ufasaha
wa lugha ipate kupendeza na kueleweka vizuri.
·
Nidhamu,
yaani adabu njema ya mzungumzaji mwenyewe asimamapo mbele za watu .
·
Mantiki
nzuri, yani mfuatano mzuri wa mawazo na fikra.
·
Sauti ya
kusikika wazi pamoja na ishara zinazoeleweka iwapo hotuba inatolewa mbele ya
watu. Ishara siyo za lazima iwapo hotuba
inatolewa kwa njia ya redio.
Hotuba zaweza kugawanywa kwa misingi mbalimbali. Baadhi ya misingi hiyo ni:
·
Urefu wa
Muda wa Matayarisho: Kulingana na uzito wa mada za hotuba zenyewe matayarisho
huwa ni ya muda mrefu kwa mada nzito, lakini huwa ni ya muda mfupi kwa hotuba
zenye mada nyepesi. Aghalabu, hotuba za dharura huwa na mada nyepesi
nyepesi, yaani zinazotolewa papo kwa papo bila ya kupata muda mrefu wa kuziandaa.
·
Aina za
Hotuba: Ziko aina nyingi za hotuba. Baadhi yake ni:
(i)
Hotuba na Mafundisho ya Kidini; aghalabu,
hizi hutolewa miskikitini, makanisani, kwa njia ya redio; lakini pia popote
penye mkusanyiko wa waumini husika.
(ii) Hotuba za Kisiasa na Kiserikali: Kwa mfano; matangazo ya taarifa za kiserikali
na chama, fafanuzi za maazimio au sheria, n.k.
(iii) Mihadhara au Masomo ya Darasani: Hizi ni hotuba au mafundisho ya Mwalinu
shuleni hasa anapofundisha kundi kubwa la wanafunzi, na hasa wanachuo wa vyuo
vikuu.
·
Nia ya
mzungumzaji katika kuzitayarisha hotuba:
Mzungumzaji
au mhutubiaji hujiwekea lengo la hotuba yake:
(i)
Kuna hotuba za kuhimiza na kualika watu
kutenda jambo fulani;
(ii) Kuna
hotuba za kupasha habari ya furaha au ya simanzi;
(iii) Kuna
hotuba za kushukuru, kukaribisha wageni,
kupongeza na kutoa hongera, kumliwaza na kumfariji mwenye huzuni na masikitiko,
(iv) Aidha, kuna hotuba za kushutumu na
kukaripia.
MAREJELEO
Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N.
(2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili,
Kidato cha 5 na 6. Aroplus
Industries Ltd: Dar es Salaam.
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu,
Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.
wazi kaka umegonga ndipo
ReplyDeletewazi kaka umegonga ndipo
ReplyDeletehiyo iko sawa
ReplyDeletekazi bora ndugu
ReplyDeletemmujaribu
ReplyDeleteAsante kwa Maelezo haya
ReplyDeleteunknown
ReplyDeleteume fanya kazi njema
ReplyDeleteInaeleweka
ReplyDelete